KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI — BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA DKT. DOROTHY GWAJIMA, WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM
YAH: UMUHIMU WA KUUPA UZITO UKATILI WA KIJINSIA MTANDAONI KATIKA MPANGO WA TAIFA DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA
Mheshimiwa Waziri,
Natumai barua hii inakukuta salama ukiendelea na majukumu yako ya kitaifa katika kuimarisha haki za wanawake, watoto, na makundi maalum nchini Tanzania. Ninatambua na kuthamini juhudi zako za kibinafsi na za Wizara yako katika kupambana na ukatili wa kijinsia, ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Nimekua shahidi wa jinsi wewe binafsi pia kutumia majukwaa ya mitandao ya jamii kupokea na kufanyia kazi malalamiko na mapendekezo mbali mbali ya wananchi, na hata nilipouliza watumiaji wa X kupitia kurasa yangu, uliongozwa kwa kutajwa na wengi — rejea hapa https://x.com/CarolNdosi/status/1864569543919579137
Ni dhahiri kwamba umejitolea kwa moyo wote kulinda na kuendeleza haki za wanawake, wasichana watoto na jamii kwa ujumla katika nchi yetu.
Binafsi, nahamasishwa pia kila unapopata nafasi namna huwa unasisitiza ushiriki wa wanaume kwenye midahalo na hata mipango ya kupingana na ukatili wa kijinsia na haki za wanawake nchini. Hata kwenye teknolojia, umeonyesha namna gani kupitia Wizara yako na Serikali ya Awamu ya 6 mmefanya jitihada za maksudi kuhamasisha ushiriki wa wanawake kwenye sekta hii, na bado tunashukuru kwa kuungana na sisi kwenye Kongamano la Wanawake na Teknolojia 2024.
Tukiwa tunaelekea kilele cha Siku ya Wanawake duniani Machi, 2025, ambayo kitaifa inafanyika Arusha, kwa namna ya kipekee ninakuja kwako kwa niaba yetu kama Taasisi ya The Launchpad/LP Digital tunaomba uliangalie kwa kina suala linalozidi kuwa tishio kubwa kwa wanawake na wasichana katika enzi hii ya kidijitali — ukatili wa kijinsia mtandaoni.
Teknolojia imeleta mabadiliko makubwa katika maisha yetu, lakini pamoja na fursa zake, imeleta changamoto mpya ambazo zinawafanya wanawake na wasichana kuwa katika mazingira hatarishi zaidi mtandaoni. Bila mfumo wa kisheria uliojumuishwa na wa kisasa, changamoto hizi, hasa zinazotokana na teknolojia zinazoibuka kama Akili Mnemba (AI) na picha za bandia (deepfakes), zitaendelea kuimarika, na kusababisha kushindwa kulinda nafasi za kidijitali dhidi ya ukatili wa kijinsia mtandaoni (Online Violence Against Women — OVAW).
Mifano Halisi ya Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni Tanzania
Tatizo hili si la kinadharia tu — limejidhihirisha kwa njia za kutisha nchini. Hapa kuna mifano kadhaa:
- Kesi za ‘Connection’ (2021- 2025)
- LP Digital Kupitia namba yetu ya dharura inayotoa msaada na ushauri wa afya ya akili na kuunganishwa na msaada wa kisheria, imepokea jumla ya kesi 245 tangu kuanzishwa kwa huduma hii, nyingi zikiwa ni za usambazwaji wa picha za utupu, na watuhumiwa wengi wakiwa ni wanaume na wenza wa waathirika. Mfano mmoja ni Tatu Shabani(sio jina halisi), mwanamitindo wa urembo mwenye umri wa miaka 20, alikumbana na kurekodiwa na uenezi wa video za faragha zake mtandaoni bila ridhaa yake. Tukio hili lilimdhuru kiakili na kuathiri hadhi yake ya kijamii. Ingawa aliripoti, uchunguzi ulichelewa, na wahusika hawakuwahi kuwajibishwa ipasavyo chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao wa 2015. Hii ilikuwa fursa ya kuweka mfano wa kisheria, lakini hatua za haraka hazikuchukuliwa.
2. Unyanyasaji wa Wanawake wa Umma na Viongozi wa Kike
- Kipindi cha uchaguzi wa 2020, wanasiasa wa kike walipokea matusi ya kijinsia, vitisho vya ubakaji, na kejeli za kimtandao. Sehemu ya 135 ya Kanuni za Adhabu inakataza unyanyasaji wa kijinsia, lakini hakuna kesi iliyofunguliwa wazi, na hivyo fursa ya kuimarisha ulinzi wa kisheria ikapotea. Hali hii imeendelea kuonekana hata hivi karibuni haswa kupitia majukwaa mawili ya Instagram na X, na tumeshuhudia hata wewe Mheshimiwa Waziri ukishambuliwa kwa matusi kudhalilishwa hata pale ulipokua unatekeleza majukumu yako.
3. Ukatili Dhidi ya Wasichana Vijana
- Ripoti za 2023 zilionyesha wasichana wanaodanganywa mtandaoni na wanaume wazima kupitia majukwaa kama WhatsApp na Mobile Application za Mahusiano yaani ‘Dating Apps’, . Kesi moja huko Mwanza ilishindwa kuendelea kwa ukosefu wa teknolojia ya uchunguzi wa kidijitali lakini pia ushirikiano wa hizi apps ambazo zinapatikana kwa urahisi pasipo kufuatilia miongozo ya usalama mtandaoni na namna gani ya kuwawajibisha watakaokiuka. Kundi la wasichana wa chuo na wasio na ajira wamekua waathirika wakubwa kutokana na changamoto za uchumi, na kurubuniwa kwa ahadi za pesa. Wengi pia wameshindwa kuchukua hatua za kisheria kutokana na woga, lakini pia uelewa wa elimu ya usalama mtandaoni pamoja na haki na wajibu wa raia wa kidijitali.
Changamoto na Fursa za Teknolojia Zinazoibuka
Mheshimiwa Waziri, teknolojia zinazoibuka kama AI na deepfakes zinawasilisha changamoto za kipekee. Deepfakes, ambazo ni video au picha bandia zinazotumia akili mnemba kuiga sura au sauti za watu, zinaweza kutumiwa kuunda maudhui ya uongo yanayowaaibisha wanawake, kuwadhalilisha, au kuwalazimisha katika vitendo visivyotakiwa.
Kwa mfano, mwanamke anaweza kuonekana kwenye video za ponografia bandia ambazo hazikuwahi kuwepo, na kusababisha madhara makubwa kiakili na kijamii. Tanzania bado haijakumbana na wimbi kubwa la deepfakes, lakini bila maandalizi ya kisheria na kiufundi, hatari hii itakuwa ngumu kuizuia haswa kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mguu wa Tanzania.
Hata hivyo, teknolojia hiyo hiyo ina fursa kubwa. Kupitia jukwaa letu la #WanawakeNaDijitali tunaendelea kutoa mafunzo ya namna gani akili mnemba inaweza kuchangia maendeleo binafsi na ya wajasiriamali. Hata hivyo, kwenye suala la Unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, AI inaweza kutumiwa kugundua na kuzuia unyanyasaji wa mtandaoni kwa uchanganuzi wa haraka wa mifumo ya vitisho au matusi kwenye mitandao ya kijamii. Hii itahitaji ushirikiano na ufuatiliaji na wamiliki na vitengo vyao ndani ya majukwa makubwa yaani ‘big tech platforms’ kama META, X, Tiktok n.k. Vile vile, inaweza kusaidia katika kampeni za uelewa na kufuatilia wahusika wa uhalifu wa kidijitali. Bila mfumo wa kisheria unaofaa, hata hivyo, hatuwezi kutumia fursa hizi kwa ufanisi, na badala yake, teknolojia itakuwa chombo cha kuongeza unyanyasaji badala ya kupunguza.
Tofauti Kati ya OGBV na TFGBV
Ni muhimu kuelewa tofauti kati ya Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni (Online Gender-Based Violence — OGBV) na Ukatili wa Kijinsia Unaochochewa na Teknolojia (Technology-Facilitated Gender-Based Violence — TFGBV):
- OGBV unahusu unyanyasaji unaofanyika kwenye mazingira ya mtandaoni pekee, kama matusi au vitisho kwenye mitandao ya kijamii.
- TFGBV ni pana zaidi, ikijumuisha matumizi ya teknolojia kuimarisha ukatili wa kimwili au kiuchumi, kama udukuzi wa akaunti za fedha za wanawake wajasiriamali au kutumia GPS kuwafuatilia waathirika(hizi kesi ziko zaidi baina ya watu walio kwenye mahusiano) hadi maeneo yao na kuwafanyia ukatili.
Tanzania inakabiliwa na aina zote mbili, lakini bila kutambua tofauti hizi katika sera na sheria, hatua zetu zitakuwa za juujuu tu. Kwa mfano, deepfakes zinaweza kuwa OGBV ikiwa zinatumika kwa kejeli mtandaoni, lakini TFGBV ikiwa zinatumika kushinikiza wanawake kulipa fidia au kuathiri maisha yao ya nje ya mtandao.
Athari za Kukosekana kwa Mfumo wa Kisheria wa Kutosha
Ingawa hamna takwimu zinaoonyesha wako wangapi haswa, Wanawake nchini Tanzania wanaongezeka kwa kasi katika matumizi ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali Wanatumia nafasi hizi kwa biashara, elimu, na uhamasishaji. Hata hivyo, tafiti zetu zinaonyesha ukatili wa kijinsia mtandaoni unaowafanya waogope kushiriki na kuwanyima fursa hizi na unaongeza pengo la kijinsia katika ulimwengu wa kidijitali. Ikiwa hatutachukua hatua, pengo hili litazidi kuongezeka, na wanawake wataachwa nyuma katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi duniani.
Mapendekezo
Mheshimiwa Waziri, ili Tanzania iwe mstari wa mbele katika kukabiliana na changamoto hizi, napendekeza hatua zifuatazo:
- Kujumuisha OGBV na TFGBV katika Mpango wa Taifa wa Kupinga Ukatili wa Kijinzi dhidi ya Wanawake na Watoto
Mpango wa Taifa unapaswa kusisitiza na kutambua aina hizi mbili za ukatili wa kijinsia na kuweka mikakati mahsusi, kama vile vitengo vya polisi vya uhalifu wa kidijitali vilivyopewa mafunzo ya AI na uchukuzi wa ushahidi wa deepfakes.
2. Kushirikiana na Wizara ya Habari na TEHAMA
Ushirikiano huu unaweza kuimarisha Sheria ya Makosa ya Mtandao wa 2015 kwa kuongeza vifungu vinavyolenga TFGBV, kama udukuzi wa faragha au matumizi mabaya ya AI, na kuunda sera zinazolinda wanawake mtandaoni.
3. Kufanya Utafiti wa Kitaifa na Kukusanya Takwimu
Utafiti unaohusisha wataalam wa teknolojia utaonyesha ukubwa wa OGBV na TFGBV, hasa hatari za Akili Mnemba, deepfakes, na kusaidia kuunda mikakati yenye ushahidi.
4. Kampeni za Uelewa kwa Umma
Kampeni zinazolenga kuelimisha jamii kuhusu hatari za teknolojia kama deepfakes na jinsi ya kuripoti visa vya OGBV na TFGBV zinaweza kuimarisha usalama wa kidijitali.
5. Kuimarisha Mfumo wa Kisheria na Upatikanaji wa Haki
Marekebisho ya sheria yanapaswa kujumuisha adhabu za wazi kwa wanaotumia AI vibaya au kueneza maudhui bandia, pamoja na kuunda vituo vya kuripoti vinavyotoa huduma za kisaikolojia na kisheria kwa waathirika.
6. Kuwekeza katika Teknolojia na Mafunzo
Kuweka vifaa vya uchunguzi wa kidijitali na kutoa mafunzo kwa polisi na mahakama kuhusu jinsi ya kushughulikia kesi zinazohusisha AI na deepfakes kutasaidia kuwapa haki waathirika kama Amida Twaha na wengine.
Mheshimiwa Waziri, huu ni wakati wa kihistoria wa kulinda wanawake na wasichana wa Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali ambao unazidi kuwa sehemu ya maisha yetu. Teknolojia inaweza kuwa chombo cha maendeleo au cha madhara, uchaguzi uko mikononi mwetu.
Bila hatua za haraka, hatari za OGBV na TFGBV zitawaacha wanawake nyuma, na kuongeza pengo la kijinsia katika uchumi wa kidijitali. Lakini kwa uongozi wako thabiti, tunaweza kugeuza hatari hizi kuwa fursa za maendeleo endelevu.
Tunaomba uchukue suala hili kwa uzito wa hali ya juu na utuongoze katika hatua za vitendo. Tuko tayari kushirikiana na Wizara yako, wataalam wa teknolojia, na wadau wengine kuhakikisha mabadiliko haya yanafanyika kwa manufaa ya jamii yetu yote.
Kwa heshima na taadhima,
Carol Ndosi
Mdau wa Teknolojia na Haki za Wanawake
Mkurugenzi wa LP Digital & Tanzania Women and Technology Association